Abstract:
Ulimwengu una lugha takribani elfu sita. Hata hivyo, nyingi katika lugha hizi zimo katika hatari ya kuangamia.
Inasemekana kwamba lugha moja ya ulimwengu huangamia katika majuma mawili. Nchini Kenya, lugha za Kisengwer,
Kisuba na Kielmolo zimo katika hatari ya kuangamia. Ingawaje lugha nyingi za ulimwengu zinakabiliwa na changamoto
za kuishi, Kiswahili kimo mbioni kukua na kupanuka. Sasa hivi, Kiswahili kimekuwa lugha ya ulimwengu na
kinatekeleza majukumu muhimu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Usambaaji wa kasi wa Kiswahili katika eneo la
Maziwa makuu Afrika unatokana na mazingira mwafaka ya ukuaji ambayo yamekuwepo tangu wakati kabla ya
ukoloni wa mataifa ya Afrika Mashariki. Makala hii inachunguza utandawazi unavyotishia uwepo wa lugha za
Kiafrika. Lugha zinazoangamia zimeanishwa katika makundi matatu - lugha zilizoangamia, lugha zilizolala na lugha
zilizo katika hatari ya kuangamia. Athari za utandawazi kwa uhai, usambaaji na matumizi ya lugha mbalimbali
ulimwenguni zimejadiliwa kwa kuangazia nyanja za elimu, uchumi, mawasiliano, siasa na hata utamaduni. Hoja
inayojengwa ni kwamba jitihada za makusudi zinapasa kutekelezwa ili kuzinusuru lugha za Kiafrika zinazokabiliwa na
tishio la maangamizi. Imebainika kwamba uhifadhi wa lugha ni muhimu kwa kuwa lugha huwasilisha utamaduni,
hutambulisha na, ni sehemu muhimu ya amali za watu.